Sunday 6 September 2015

Mapungufu ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015

Mapungufu Yaliyomo Kwenye Ilani Ya Uchaguzi Ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ya 2015 - 2020 Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 – 2020, chama kinachotawala na kinachotaka kiendelee kutawala haiongelei chochote juu ya ilani iliyopita, jinsi ilivyopaswa kutekelezwa, wapi ilifanikiwa na wapi haikufanikiwa na haielezei ni kwanini haikufanikiwa na badala yake CCM wanakuja na ilani mpya ya moja kwa moja utadhani ndo wanataka kuingia madarakani kwa mara ya kwanza.

Katika ilani yao CCM wanasema kuwa chini ya utawala wao watanzania wamepata mafanikiao makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii, lakini hawajatwambia haya mafanikio ni makubwa kulinganisha na yapi, yaliyopita? Yaliyotarajiwa au inavyopaswa kuwa kwa mtizamo wao?

Katika ilani yao, bado wanaongelea kupunguza tatizo la ajira na hasa kwa vijana. Hapa wameshashindwa kuondoa tatizo hilo kabla ya kuanza kutekeleza ilani yao maana wanaongelea kupunguza badala ya kulimaliza kabisa ili kama ikitokea wakashindwa kulimaliza, basi watalipunguza kwa kiasi kikubwa. Sasa kama lengo ni kupunguza, basi wakishindwa litapungua kwa kiasi kidogo tu. Na wanaongelea kupunguza tatizo hili la ajira kwa vijana pekee na sio rika lingine la Watanzania.


Ilani ya CCM inaongelea juu ya kuwawezesha wafanyabiashara ndogo kupata mikopo nafuu na kuwapatia maeneo ya kudumu ya kufanyia biashara zao. Hapa kwanza ilani ya chama kinachotawala itueleze kwanza ni kwanini imekuwa ikiwafukuza na kuwanyang’anya vitendeakazi pamoja na bidhaa zao hawa wafanyabisahara wadogo katika miji yetu, na nikwanini sasa inafikiri ni wakati wa kuwatambua hawa wafanyabiashara, maeneo mazuri ya kufanyia biashara na kuhakikisha wanapata mikopo nafuu na nikwanini haipangi kuwawezesha hata ikibidi kwa kuwapa ruzuku wafanyabiashara hawa ili wawe wafanyabisahara wakubwa na ikibidi wakatafute masoko nje ya nchi.

Kilimo Kwanza. Ilani ya CCM inasema kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao. Ilani hiyo haielezei itafanya nini ili kuhakikisha wakulima wanatafuta masoko popote pale na kuuza mazao yao kwa bei ya juu au bei shindani. Ikizingatiwa serikali yake (CCM) imekuwa ikiwazuia wakulima kuuza mazao nje ya nchi kwenye bei kubwa na kuwalazimisha kuuza mazao kwa bei ya chini inayopangwa na serikali na vyama vya ushirika kwa mfano zao la kahawa kule mkoani Kagera lenye bei ya juu nchi jirani kule Uganda au wakulima wa Mahindi wanaozuiwa kuuza Mahindi yao katika nchi zilizotuzunguka.

Pia wakulima wamekuwa wakinyonywa chini ya serikali ya CCM kwa kulazimika kuuza mazao yao kwa kupitia madalali ambao huwanyonya wakulima kwa kutangaza bei ndogo sana huku wakiuza kwa bei ya juu ya kupata faida kubwa kuliko wakulima wanaowekeza nguvu zao kubwa sana. Ilani itueleze ni kwanini imeruhusu unyonywaji huu kwa wakulima na itafanya nini kuuondoa endapo itapewa ridhaa ya kuendelea kuliongoza taifa hili.

Ajira kwa vijana. Ilani ya CCM inasema kuwa mafanikio katika upanuzi wa elimu ya Sekondari na Vyuo yameongeza mahitaji ya ajira ya vijana wasomi kila mwaka ikilinganishwa na nafasi zinazokuwepo. Hapa swali ni je, nafasi zinazokuwepo wapi? Si kila ilani ya uchaguzi huahidi kuzalisha ajira mpya? Pia inaonekana mafanikio iliyoyaleta CCM ya kupanua elimu ya sekondari na vyuo yamekuwa mwiba kwake kwa kuongeza tatizo kubwa la ajira na upanuzi huu wa elimu basi umefanyika ghafra, haukutegemewa ndo maana ukazalisha tatizo la ajira.

Pia hapa CCM inatumia kigezo cha utafiti cha Taasisi ya Takwimu (NBS) kuhusu ajira kinachosema kuwa mtafuta ajira ni Yule mwenye elimu au vyeti anayetafuta ajira na kwahiyo wale watanzania ambao hawajasoma hawapaswi kuajiriwa na wao sio sehemu ya tatizo la ajira kwa serikali iliyoko madarakani.

Rushwa. Ilani ya CCM ya 2015 – 2020 inaonekana kukerwa sana na tatizo la rushwa na kutoa ahadi nzito za kupambana nayo kamailivyo kwa ilani zilizopita lakini haiweki wazi ni kwanini rushwa imeendelea kushamiri na kwanini wamekuwa wakionekana kushughulikia rushwa ndogo ndogo zaidi. Pia ilani haisemi ni kwanini watuhumiwa wa rushwa kubwakubwa huwa wanaonekana kushinda kesi hata wale wanaoshindwa kesi, adhabu zao zinalalamikikwa kuonekana kuwa ndogo kuliko makosa. Je tutegemee kupambana na rushwa kwa dhati hapa?

Ulinzi na usalama. Ilani ya CCM ya 2015 -2020 inahaidi kuwalinda watanzania. Ilani hii haionyeshi kuwa uhasama kati ya walinda usalama na raia wema iko mashakani. Haisemi ni kwa jinsi gani itakomesha vitendo vya askari wetu kuwapiga, kuwamwagia maji yenye kemikali, mabomu ya machozi n.k raia wema wasionasiraha. Tumeona wafanyabiashara ndogondogo, wafuasi wa vyama vya upinzani na wanafunzi hasa wale wa elimu ya juu wanavyopigwa, kutiwa ulemavu na hata kudhalilishwa na walinda usalama.

Pia majambazi na wahalifu wanatamba sana kiasi cha kuzuia vyombo vya usafiri kushindwa kuendelea na safari zao hasa nyakati za usiku. Ilani haionyeshi ni kwa kiasi gani itashughulika nao hawa. Maasikari wetu hawa pia wamekuwa wahanga wa wahalifu, majangili au tuwaite magaidi ambao wameendelea kuwateka, kuwauwa na kuwanyang’anya vitendea kazi vyao. Ilani ya uchaguzi inapaswa kuelezea pasi na shaka ni kwa jinsi gani itashughulikia ushenzi huu na kurudisha heshima ya jeshi letu la polisi na taifa kwa ujumla.

Uchumi

Ilani ya CCM ya mwaka 2015 – 2020 inasimamia kukua kwa uchumi wa taifa umekuwa ni mzuri na wa kuridhisha yaani wa asilimia 7. Hiki nikigezo jumla ambacho hakionyeshi uhalisia wa ukuaji au kutokukua kwa uchumi wetu. Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa uchumi kama hauendani na maendeleo ya mtu mmoja mmoja basi hauna maana.

Ni kweli kuwa uchumi wetu unakua lakini pia pato au uchumi wa mtu mmoja mmoja limeendelea kuwa dogo na kimsingi mtu mmoja mmoja ameendelea kuwa masikini. Ilani haielezi jambo hili na haionyeshi itafanya nini kushughulikia uchumi wa mtu mmoja mmoja ili kujenga uchumi unaowanufaisha watu wote.

Ilani inasema kuwa itahakikisha deni la taifa linaendelea kuwa stahimilivu bila kutwambia ni sababu gani zilizofanya deni hili kupaa kutoka trillion 10 mwaka 2005 hadi zaidi ya trilioni 35 mwaka 2015 ili tuone kama kweli inaweza kulidhibiti.

Ilani haitoi mwelekeo wowote wa kuonyesha ni kwa jinsi gani itahakikisha inaanzisha na kusaidia biashara za vijana wa kitanzania kukua na kwenda mpaka nje ya mipaka yetu ili kujiingizia vipato, kulipa kodi na kuliingizia taifa letu fedha za kigeni. Pia haitoi maelezo yoyote juu ya nafasi ya Tanzania na jinsi ya kushindana katika masoko ya nje kwa kuanzia na yale ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADEC n.k na hivyo kusababisha taifa letu kubakia nyuma katika masoko hayo endapo Watanzania wataipatia tena CCM ridhaa ya kuwaongoza tena miaka mingine mitano.

Pia ilani hiyo haitoi maelezo ya kina juu ya matumizi ya rasilimali yetu kwanza kuhakikisha mapato yanakuwa makubwa zaidi na kutafuta vyanzo vipya vya rasilimali zetu hizi. Wala hawasemi watafanya nini kuhakikisha wafanyabiashara wakubwa wanabanwa ili waaache kukwepa ulipaji kodi kwa kusingizio cha likizo ya kodi (tax holidays) na ni jinsi gani itawasaidia wajasiliamali wadogo kupata misamaha dhidi ya kodi zinazoweza kuwasababishia kushindwa kuendeleza biashara zao.

Ubaguzi katika huduma. Ilani hii ya CCM ya 2015 – 2020 haiongelei chochote kuhusu kuimarisha huduma zote muhimu na kuwahudumia wananchi wote kwa usawa. Kwa mfano huduma ya umeme imekuwa ni ya kusuasua miaka yote na hufikia wakati umeme unapatikana kwa mgawo. Katika mikoa yote, kuna maeneo ya “wakubwa” ambayo ni nadra sana huduma za umeme na maji kutokupatikana mahala pote.

Pia ilani haionyeshi jinsi ya kuondoa ubaguzi wa mchakato wa kupata ajira katika Utumishi wa Umma. Ilianzishwa Sekretariet ya Ajira katika Utumishi wa Umma ambayo utangaza kazi, huendesha usaili na kuita kazini wale waliofanikiwa kupata ajira. Sekretariati hii huwajali zaidi waombaji kazi waishio Dar salaam na mikoa ya jirani kwani saili zake karibia zote huzifanyia Dar es salaam na kwahiyo ili mtu ashiriki mchakato wa kushindana kupata ajira serikalini ni vyema akawa anaishi Dar. Lakini kama mtafuta ajira huyu anaishi mikoa kama ya Kigoma, Kagera au Mara, basi aachane na mchakato huo au awe tayari kulipa gharama za nauli za zaidi ya shilingi milioni moja za usafiri na malazi ili akajaribu bahati yake.

Kuhusu maji, ilani ya CCM inadai kuwa itapunguza tatizo hilo kutoka asilimia 53.4 kwa wakazi wa vijijini hada asilimia 70. Sekta muhimu kama hii ambayo inawezesha kilimo na kuokoa nguvu kazi ya wananchi kutumia muda na nguvu nyingi kufuata tu maji, kwanini isilengwe kumalizwa kabisa kwa asilimia miamoja? Hizo asilimia 70 anabakiziwa nani? Bila kuona haya, ilani inasema kuwa itaendelea kujenga vituo vya kuchotea maji badala ya kuhakikisha maji yanamfikia mwananchi pale alipo. Hapa ndo kuna aibu ya kuona viongozi wetu kama vile Rais, waziri na viongozi waandamizi wanazindua miradi ya maji kwa kuwatwisha ndoo wakinamama katika karne hii.

Wakati magonjwa ya mulipuko yakiendelea kutuumiza na kuondoa maisha, ilani ya CCM inasema kuwa itaongeza kasi ya ujenzi wa miundombinu ya maji taka na sio kusimamia na kuhakikisha serikali yake (kama itapata ridhaa) inamalizia kabisa miundombinu hiyo haraka sana iwezekanavyo ili kuepusha wananchi na magojwa ya mulipuko, harufu mbaya na kupendezesha miji yetu.

Hayo ndiyo mapungufu makubwa ambayo wagombea wa CCM wanapaswa kuyatolea ufafanuzi kwa wapiga kura, waseme kama waliyasahau au si vipaumbele au yatatekelezwa bila kulazimikwa kuandikwa katika ilani yao hiyo

Kamala J Lutatinisibwa.
0754771601
jlkamala@gmail.com

No comments: